Monday, 20 March 2017

KUTENGENEZAJI WA VYAKULA VYA KUKU

UTENGENEZAJI WA VYAKULA VYA KUKU

JINSI YA KUPATA VIRUTUBISHO MBALIMBALI

Ili kifaranga awe na afya nzuri na akue upesi anahitaji chakula maalumu.  Chakula hicho ni mchanganyiko wa viini lishe mbalimbali.  Kila kiini lishe ni lazima kiwe katika kiwango sahihi kulingana na mahitaji ya mwili wa kifaranga.  Viini lishe anvyohitaji kifaranga ni:
👉 Wanga   👉Mafuta
👉 Protini  👉 Vitamini
👉 Madini    👉 Maji

Mchanganyiko sahihi wa viini lishe kwa mahitaji ya kifaranga, humuwezesha kukarabati na kujenga mwili (kukua) haraka.  Viini lishe viini lishe vilivyotajwa hapo juu hupatikana katika aina mbali mbali za viungo ghafi vya chakula cha kuku kama ifuatavyo:
🐣 Mtama wa aina tofauti
🐣 Karanga
🐣 Mahindi

WANGA
Wanga hupatikana katika pumba, chenga au dona ya nafaka kama mahindi au mtama aina ya serena, lulu nk.

VYANZO VYA WANGA

MAFUTA

Mafuta hupatikana katika mbegu kama karanga au alizeti.  Mbegu hizi zikikamuliwa mashudu yake hubaki na kiasi fulani cha mafuta.  Haya hutumika kulishia mifugo mbalimbali.
🐥 Alizeti
🐥 Mashudu ya karanga
🐥 Mashudu
🐥 Dagaa

PROTINI

Kiini lishe hiki hupatikana katika mashudu ya karanga, au alizeti, dagaa, damu ya wanyama kama ng'ombe, mbuzi nk.

Damu hiyo unaweza kuipata machinjioni.  Changanya damu mbichi na pumba katika ndoo au chombo chochote kilicho wazi upande mmoja.  Vuruga mchanganyiko huo kwa kipande cha mti, halafu fikicha kwa viganja ili kuondoa mabonge.  Sambaza mchanganyiko huu juu ya bati halafu anika juani mpaka ukauke kikamilifu.

Tahadhari: Ukiamua kutumia damu katika mchanganyiko wa chakula hakikisha utaitumia mfululizo.  Maana kuku wakishaanza kuizoea ikikosekana huanza tabia ya kudonoana.

Protini hupatikana pia katika unga wa mbegu za jamii ya kunde kama maharage, kunde,soya nk.

MADINI

Madini aina ya 'Calcium' na fosforasi hupatikana katika unga wa dagaa na mifupa ya wanyama iliyochomwa na chokaa maalumu ya kuku ipatikanayo katika maduka ya pembejeo za kilimo, chumvi, hata majivu ya kawaida ya jikoni.

MANDALIZI YA UNGA WA MIFUPA

Chukua mifupa ya wanyama hasa ile mirefu (ya miguu na mingineyo) ichome moto hadi iive.  Utafahamu kuwa imeiva inapokuwa na rangi nyeupe mifupa mizuri zaidi ni ile mirefu yaani miguu na mikono kuliko ile ya kichwa ambayo mara nyingi huwa kama mkaa (ambayo haifai).  Iache ipoe kabisa halafu itwange hadi isagike iwe unga.  Hapo inakuwa tayari kuchanganywa kwenye chakula cha kuku wako.

VITAMINI

Vitamini hupatikana katika majani mabichi ya mti aina ya Lucina, majani ya mpapai, mchicha wa nyumbani au wa porini.

Vitamini hupatikana pia katika majani mabichi ya mimea ya jamii ya mikunde kama marejea na luseni nk. Ambayo hupendelea kuliwa na kuku.  Unaweza kukausha mimea hiyo kivulini na kuitwanga katika kinu au kufikisha kwa viganja ili kupata unga.
Viungo ghafi vilivyotajwa hapo juu hupatikana katika vijiji vingi hapa nchini.  Kwa hiyo mkulima unaweza kujitengenezea mwenyewe chakula kinachofaa kwa ajili ya kuku wako.

MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIA KATIKA KUANDAA CHAKULA CHA KUKU

🐤 Upatikanaji wa malighafi kama:- Mahindi, mtama, pumba, nk.  Kutegemeana na kinachopatikana katika eneo husika.

🐤 Uchaguzi wa malighafi utategemea uwezo wa mfugaji

🐤 Utengenezaji wa chakula unategemea rika la kuku unaowatengenezea.

🐤 Kiasi au wingi wa chakula kitakachotengenezwa kitategemea uwezo wa mfugaji kifedha.

🐤 Malighafi zinazotumika kutengenezea chakula ziwe zimekauka vizuri ili kuepuka uwezekano wa kuota ukungu ambao ni hatari kwa afya ya kuku.

🐤 Hata kama malighafi ni kavu ikaguliwe kuhakikisha kwamba haina ukungu na iwe haijaoza

MATAYARISHO

🐓 Andaa aina zote za viungo ghafi zilizo bora katika wingi wa kutosha (uzito).  Pumba au dona, mashudu nk. Viwe havikuvunda.  Tena viwe safi yaani havikuchanganyika na uchafu wowote bila kushambuliwa na wadudu.

🐓 Tayarisha kopo tupu lenye ujazo wa lita 1 kwa ajili ya kupimia.  Mfano wa kopo linalofaa ni lile la Pride, Kimbo, au Blue Band.  Kila kiungo unachotaka kuchanganya pima ujazo wa lita moja ili ujue una uzito gani (waweza kuomba msaada maduka ya jirani wakupimie).  Ukishafahamu hivyo utaweza kupima uzito sahihi wa kuweka kwenye mchanganyiko wako.  Kwa mfano kama lita 1 ya pumba ni nusu kilo, ina maana mahali unapotakiwa kuweka kilo 1 utaweka lita 2 yaani makopo 2 ya lita 1.

🐓 Kama unaandaa kiasi kikubwa cha chakula ni vizuri uwe na mizani ya kutumia kwaajili ya kuandaa chakula chenye uwiano sahihi.  Maana ni rahisi kupoteza hesabu za makopo kama unaandaa chakula kingi.

🐓 Kama mchanganyiko wako wa chakula una dagaa, mahindi, au mashudu hakikisha kwamba vitu hivi vinabarazwa mashineni kabla ya kuchanganya (yaani vinavunjwa vunjwa).

🐓 Baraza vyakula hivi upate chembechembe zinazolingana na rika ya kuku unaotaka kulisha chakula unachoandaa.

UTARATIBU WA KUCHANGANYA VIUNGO GHAFI

Kwanza pima kwa makopo au mizani viungo vyote vyenye uzito mkubwa viweke kwenye fungu lake moja na kuvichanganya vizuri.  Kwa mfano:
🐧 Unga wa nafaka
🐧 Pumba ya mashudu
🐧 Mashudu ya alizeti

Halafu kwenye fungu la pili changanya vizuri viungo vyenyee uzito mdogo kama:

🐦 Unga wa dagaa
🐦 Unga wa mifupa au chokaa
🐦 Chumvi ya jikoni

MWISHONI changanya mafungu yote mawili kikamilifu.

KUTENGENEZA CHAKULA CHA VIFARANGA UMRI WA SIKU YA KWANZA HADI MAJUMA NANE (0-8 WIKI)

Unga wa nafaka, mahindi au mtama kilo 40
Pumba za mtama, mahindi na uwele kilo 27
Mashudu ya alizeti, ufuta karanga au pamba nk kilo 20
Unga wa mifupa au chokaa ya kuku kilo 2.25
Dagaa au mabaki ya samaki kilo 10
Chumvi ya jikoni kilo 0.5
Virutubisho (Premix) kilo 0.25

Jumla kilo 100

No comments:

Post a Comment

COMMENTS/MAONI AU USHAURI

MATANGAZO