Saturday, 5 January 2019

PSYCHOLOGY: SAIKOLOJIA DALILI 7 KUWA MKEO ANAHITAJI UMSIKILIZE

PSYCHOLOGY: SAIKOLOJIA DALILI 7 KUWA MKEO ANAHITAJI UMSIKILIZE


PSYCHOLOGY: SAIKOLOJIA DALILI  7 KUWA MKEO ANAHITAJI UMSIKILIZE
Wakati fulani kitu pekee ambacho mwanamke anakihitaji ni mtu wa kumsikiliza. Njia maridhawa ya kumsaidia mkeo katika
matatizo yake, kwanza ni kumsikiliza na kumakinika kwa anachosema kisha utoe maoni yako juu ya suluhisho la tatizo husika iwapo ataomba ufanye hivyo.
Iwapo hutambui ujumbe ambao mkeo anajaribu kuutuma, basi Famasia ya Ndoa Maridhawa inakuletea ishara saba za wazi zinazoonesha kuwa mkeo anahitaji sana umsikilize:

1. ANAPOONESHA TABASAMU AMBALO SIO HALISI:
Mwanamke anayeweza kutabasamu hali ya kuwa hajisikii vizuri, basi huyo ni mwanamke madhubuti, lakini bado anahitaji faraja yako. Mkumbatie na umuombe afunguke.
2. IWAPO SIKU NZIMA ALIKUWA PEKE YAKE NA WATOTO
Anahitaji kupata mazungumzo ya mtu mzima. Kama ni mama wa nyumbani, bila shaka atakachokuwa akikisikia kwa siku nzima ni makelele ya watoto, vilio vyao na sauti za vipindi vya katuni. Unaporudi nyumbani muulize kuhusu siku yake ilivyokuwa ili kumpa mazungumzo ya kiutu-uzima ambayo alikuwa na shauku nayo kwa kutwa nzima.
3. ANAPOKUWA KIMYA KULIKO KAWAIDA
Anapokuwa na ukimya usiokuwa wa kawaida, anaweza kuwa na hasira au msongo. Mkumbatie na umuulize kinachoendelea akilini mwake.

4. ANAPOSEMA KWA HASIRA "SAWA"
Iwapo uko kwenye ndoa kwa muda mrefu au unazifahamu silika za wanawake, anaposema "sawa" yaweza kumaanisha "sio sawa". Yumkini tatizo lisionekane, lakini huhitaji kuchimbua kutafuta mzizi wa tatizo. Muulize tu mambo gani hayako sawa na namna unavyoweza kusaidia kuyaweka sawa. Atapenda sana kuona kuwa unajali sana hisia zake.

5. ANAPOKUWA KATIKA MOOD NZURI
Anataka umsikilize anapokuwa na furaha kwa kiwango kilekile anachotaka umsikilize anapokuwa na huzuni. Muulize kuhusu siku yake ilivyokuwa. Yumkini anatamani kukupa habari njema.

6. ANAPOCHOSHWA NA MAJUKUMU YA KUTWA NZIMA
Tengeneza utayari wa kumsikiliza pindi anapokuwa na siku iliyojaa majukumu kayaya. Mkumbushe namna unavyothamini yote anayoyafanya kwa ajili yako na familia yenu pia. Hatua hii maridhawa itamthibitishia kuwa yote anayoyafanya yanaonekana na kumpa hamasa ya kuendelea kufanya mambo mazuri na kujituma zaidi.

7. ANAPOJIANDAA KULALA
Tengenezeni mazingira na utaratibu wa kuzungumza kabla ya kulala. Mweleze namna siku yako ilivyokuwa na usikilize upande wake pia. Muda huu wa ukuruba huwaleta pamoja kihisia, na atafurahia kutumia dakika hizo za mwisho kuzungumza nawe.
Kaka yangu, zichunguze ishara zinazoonesha kuwa mke anahitaji umsikilize. Anahitaji uwe pembeni yake anapokuwa na msongo au anapokuwa na furaha. Aidha, kwa upande wako pia, kama unataka mkeo akusikilize, mwambie. Ndoa yenye afya huimarika zaidi pindi wanandoa wanapokuwa na uwazi, ukweli na wakawa tayari kusikiliza.

No comments:

Post a Comment

COMMENTS/MAONI AU USHAURI

MATANGAZO