UTUNZAJI WA NG’OMBE WAKUBWA
Kundi hili linajumuisha ng’ombe wenye mimba, wanaokamuliwa na madume. Mfugaji anapaswa kutunza vizuri ng’ombe wake wakubwa kwa lengo la kumpatia malisho bora na maji safi ya kutosha kila siku. Mambo muhimu ya kuzingatia katika utunzaji wa ng’ombe wakubwa ni pamoja na:-
- Ng’ombe apatiwe majani makavu (hei) wastani wa kilo 10 au majani mabichi kilo 40 kwa siku kutegemeana na uzito. Iwapo malisho hayatoshi hususan wakati wa kiangazi apewe masalia ya mazao (viwandani na mashambani) kama molasisi, mabua, maharage, mpunga n.k
- Ng’ombe apewe vyakula vya ziada (pumba, mashudu, madini mchanganyiko, unga wa mifupa na chokaa) kulingana na hatua na kiwango cha uzalishaji na
- Ng’ombe apatiwe kinga na tiba ya magonjwa kulingana na ushauri wa mtaalam wa mifugo.
UPANDISHAJI
Mfugaji anapaswa kumpandisha ng’ombe kwa umri na wakati muafaka ili kuepuka matatizo ya uzazi na pia kuhakikisha anapata ndama bora na maziwa mengi. Mambo muhimu ya kuzingatia ni pamoja na
- Mtamba apandishwe akiwa na umri wa miezi 17 -24 na uzito wa kilo 230 – 300 kwa ng’ombe wa kigeni na umri wa miezi 30 – 36 na uzito wa kilo 200 kwa ng’ombe wa asili.
- Ng’ombe aliyekwisha zaa apandishwe siku 60 baada ya kuzaa na
- Siku 18 – 23 baada ya kupandishwa, ng’ombe achunguzwe kama ana dalili za joto ili apandishwe tena. Iwapo ng’ombe ataendelea kuonyesha dalili za joto baada ya kupandishwa mara tatu mfugaji apate ushauri wa mtaalam wa mifugo.
UMRI NA UZITO UNAOSHAURIWA KUPANDISHA MTAMBA
AINA YA NG’OMBE
UZITO (KG)
UMRI (MIEZI)
Friesian
240 – 300
18 – 24
Ayrshire
230 – 300
17 – 24
Jersey
200- 250
18 – 20
Mpwapwa
200 – 250
18 – 20
Chotara
230 – 250
18 – 24
Boran
200 – 250
24 - 36
Zebu
200
30 -36
DALILI ZA NG’OMBE ANAYEHITAJI KUPANDWA
Ni muhimu mfugaji akazitambua dalili za ng’ombe anayehitaji kupandwa ili aweze kumpandisha kwa wakati. Dalili hizo ni pamoja na
§ Kupiga kelele mara kwa mara
§ Kutotulia/kuhangaika
§ Kutokwa na ute mweupe usiokatika ukeni
§ Kupenda kupanda wenzake na husimama akipandwa na wenzake na
§ Kunusanusa ng’ombe wengine
Ng’ombe akionyesha dalili za joto apandishwe baada ya masaa 12, kwa kuhimilisha au kwa kutumia dume bora (kwa mfano, akionyesha dalili asubuhi apandishwe jioni na akionyesha dalili jioni apandishwe asubuhi).
UHIMILISHAJI
Uhimilishaji ni njia ya kupandikiza mbegu kwa ng’ombe jike kwa kutumia mrija. Faida za uhimilishaji ni pamoja na kusambaza mbegu bora kwa haraka na kwa gharama nafuu, kupunguza gharama za kutunza dume na kudhibiti magonjwa ya uzazi.
ILI MFUGAJI ANUFAIKE NA HUDUMA HII ANAPASWA KUFANYA YAFUATAYO:-
- Kuchunguza kwa makini ng’ombe mwenye dalili za joto
- Kumjulisha mtaalam wa uhimilishaji mapema ili kuwezesha zoezi hili kufanyika kwa wakati.
- Kuchunguza kama ng’ombe atarudi kwenye joto siku ya 18 – 23 baada ya kupandishwa na
- Ng’ombe aliyepandishwa apimwe mimba siku 60 hadi 90 baada ya kupandishwa.
MATUNZO YA NG’OMBE MWENYE MIMBA
Ng’ombe mwenye mimba huchukua miezi 9 hadi kuzaa. Katika kipindi hicho chote anastahili kupatiwa lishe bora na maji ya kutosha ili akidhi mahitaji ya ndani aliye tumboni na kutoa maziwa mengi baada ya kuzaa.
Mambo ya kuzingatia ni pamoja na
- Ng’ombe apewe lishe bora na maji ya kutosha kipindi chote cha mimba
- Miezi 2 kabla ya kuzaa apewe kilo 2 za chakula cha ziada kwa siku
- Apewe kinga dhidi ya maambukizi na tiba ya magonjwa
- Ng’ombe anayekaribia kuzaa, hususani mtamba, azoeshwe kuingia kwenye sehemu ya kukamulia.
DALILI ZA NG’OMBE ANAYEKARIBIA KUZAA
Mfugaji anapaswa kufahamu dalili za ng’ombe anayekaribia kuzaa ili aweze kufanya maandalizi muhimu. Dalili hizo ni pamoja na
Kujitenda kutoka kwa wenzake
Kiwele kuongezeka
Chuchu kutoa maziwa zikikamuliwa
Kutokwa na ute mwekundu na sehemu za uke kuvimba na kulegea
Kuhangaika kulala chini na kusimama na
Kati ya saa moja hadi mbili kabla ya kuzaa sehemu ya uke hutokwa na maji mengi ambayo husaidia kulainisha njia ya ndama kupita.
HUDUMA KWA NG’OMBE ANAYEZAA
Ng’ombe anayezaa anahitaji uangalizi wa karibu ili kuhakikisha usalama wa ng’ombe na ndama anaezaliwa. Mambo ya kuzingatia ni pamoja na yafuatayo:-
- Sehemu ya kuzalia ng’ombe iandaliwe kwa kuwekwa nyasi kavu na laini na iwe safi.
- Ng’ombe ahamishwe sehemu iliyoandaliwa kwa ajili ya kuzaa mara baada ya dalili za kuzaa kuonekana na
- Ng’ombe aachwe azae mwenyewe bifa usumbufu
MFUGAJI APATE USHAURI/HUDUMA KUTOKA KWA MTAALAM IWAPO MATATIZO YAFUATAYO YATAJITOKEZA:-
- Ng’ombe kushindwa kuzaa kwa masaa mawili hadi matatu baada ya chupa kupasuka
- Kondo la nyuma kushindwa kutoka masaa sita baada ya kuzaa
- Kizazi kutoka nje na
- Ng’ombe kushindwa kusimama baada ya kuzaa
MATUNZO YA NG’OMBE ANAYEKAMULIWA
Ng’ombe anayekamuliwa anahitaji kupata chakula kwa ajili ya kujikimu na cha ziada kwa ajili ya uzalishaji wa maziwa. Ili kukidhi mahitaji ya uzalishaji wa maziwa ng’ombe
v Apewe chakula cha ziada kwa kiwango cha kilo 1 kwa kila lita 2 – 3 za maziwa anayotoa.
v Apewe madini na virutubisho vingine kulingan ana mahitaji
v Apewe maji mengi kwa vile ni ya muhimu katika kutengeneza maziwa.
v Aachwe kukamuliwa siku 60 kabla ya kuzaa. Uachishwaji huu ufanywe taratibu ili ifikapo siku ya 60 kabla ya kuzaa ukamuaji usitishwe.
v Baada ya kusitisha kukamuliwa apewe kilo 2 za chakula cha ziada kwa siku hadi atakapozaa na
v Apatiwe kinga dhidi ya maambukizi ya magonjwa na tiba kulingana na ushauri wa mtaalam wa mifugo
No comments:
Post a Comment